Hamas yadai kuhusika na mlipuko wa bomu Israeli
Hamas yadai kuhusika na mlipuko wa bomu Israeli

Kundi la Hamas limedai kuhusika na mlipuko wa bomu mjini Tel Aviv siku ya Jumapili usiku, huku mamlaka ya Israeli ikisema ilimuua mshukiwa wa shambulizi hilo na raia mmoja akajeruhiwa.
Taarifa kutoka kundi hilo lenye silaha ilisema ilikuwa ni "operesheni ya mauaji" iliyofanywa kwa ushirikiano na kundi la Palestina Islamic Jihad.
Pia imeonya kwamba mashambulizi ya kujitoa mhanga "yatarejea" ikiwa Israeli itaendelea na kile ilichokiita "mauaji" ya Wapalestina.
Jeshi la polisi la Israeli na huduma ya usalama ya ndani ya Shin Bet walisema mapema kwamba wanaweza kuthibitisha kuwa hilo ni shambulio la kigaidi lililohusisha kilipuzi kibaya.
Mlipuko huo ulitokea katika mtaa wa Lehi kusini mwa Tel Aviv, takriban saa moja baada ya waziri wa mambo ya nje wa Marekani kutua mjini humo kushinikiza kusitishwa kwa mapigano huko Gaza na kuachiliwa kwa mateka.
Kanda za CCTV zilizorekodiwa muda mfupi kabla zilionekana kumuonyesha mwanamume wa makamo akipita karibu na duka akiwa amebeba begi mgongoni.
Huduma ya Israeli ya Magen David Adom ilisema kuwa wahudumu wa afya walimpata mwanamume aliyepoteza fahamu katika miaka yake ya 50 akiwa na majeraha mengi na kutangaza kuwa amefariki dunia katika eneo la tukio.
Mtu mmoja, 33, aliyekuwa akitazama alijeruhiwa na vipande vya bomu mikononi na kifuani na kutibiwa na wahudumu wa afya kabla ya kupelekwa katika hospitali ya eneo hilo.
"Ilikuwa muujiza kwamba halikulipuka katika sinagogi la karibu au katika eneo la kufanya manunuzi. Lingesababisha makumi ya vifo," Kamanda wa Polisi wa Wilaya ya Ayalon Haim Bublil alisema Jumatatu, kulingana na gazeti la Jerusalem Post.
Utambulisho wa mhalifu huyo bado haujajulikana, lakini polisi wanashuku alikuwa Mpalestina.
Comments
Post a Comment